Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru kitaifa asifu kiwanda cha uzalishaji na usambazaji wa nguzo za zege.

Bagamoyo, Tanzania | 18 April 2026

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Wazo Mwang’onda, ametembelea na kukagua kiwanda cha nguzo za zege cha Coast Concrete Poles Ltd kilichopo Bagamoyo, akieleza kuwa uwekezaji huo ni suluhisho muhimu la kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji miti.

Akizungumza Aprili 18, 2026, wakati Mwenge wa Uhuru ulipopitia miradi nane katika wilaya hiyo, Mwang’onda alisisitiza kuwa mradi huo unachangia kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira pamoja na kukuza uchumi wa viwanda nchini. Aidha, aliwapongeza wawekezaji wa ndani kwa juhudi zao na kuwahamasisha kuongeza uzalishaji pamoja na kupanua masoko ndani na nje ya nchi.

 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bridget Temba, alieleza kuwa kampuni hiyo ni tanzu ya DERM Group, iliyoanzishwa mwaka 2018 kupitia ubia na kampuni ya Foshan Nanhai kutoka China. Alibainisha kuwa mradi huu unalenga kuzalisha nguzo za zege zinazoweza kuokoa takribani miti 98,000 kila mwaka.

Ameongeza kuwa uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 10 umewezesha kiwanda hicho kuzalisha wastani wa nguzo 266 kwa siku, zinazotumika katika miradi ya taasisi mbalimbali kama TANESCO, TTCL na REA, pamoja na sekta binafsi. Hadi sasa, jumla ya nguzo 150,000 zimesambazwa.

Aidha, kiwanda hicho kimetoa ajira zaidi ya 300 kwa Watanzania, ambapo asilimia 80 ni wakazi wa Bagamoyo. Mradi wa upanuzi uliopo umefikia asilimia 80, na ukikamilika utaongeza uzalishaji hadi nguzo 466 kwa siku pamoja na kuunda ajira mpya 250.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, alibainisha kuwa jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 11.4 imekaguliwa na mingine kuwekewa mawe ya msingi katika kipindi cha Mbio za Mwenge wa Uhuru wilayani humo.

 

Posted in
All

Post a comment

Your email address will not be published.